1 Siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
2 “Wewe mtu! Mgeukie Farao mfalme wa Misri, utoe unabii juu yake na nchi yote ya Misri.
3 Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Mimi nitapambana na wewe mfalme wa Misri,wewe mamba ulalaye mtoni Nili!Wewe unafikiri kwamba Nili ni wako,kwamba wewe ndiwe uliyeufanya!
4 Basi, nitakutia ndoana tayani mwako,na kufanya samaki wakwame magambani mwako.Nitakuvua kutoka huko mtoni.
5 Nitakutupa jangwani,wewe na samaki hao wote.Mwili wako utaanguka mbugani;wala hakuna atakayekuokota akuzike.Nimeutoa mwili wakouwe chakula cha wanyama wakali na ndege.
6 Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.“Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete.
7 Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao.