10 “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda.
11 Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake.
12 Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”
13 Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25.
14 Sehemu ya madhabahu itakayokuwa chini kabisa tokea juu ya msingi itakuwa na kimo cha mita 1. Sehemu itakayofuata itawekwa nyuma kutoka kwenye ukingo sentimita 50 kuzunguka, na kimo cha mita 2. Sehemu itakayofuata nayo itawekwa nyuma ya ukingo sentimita 50 kuzunguka.
15 Sehemu hii ya juu, ambayo itatumika kuteketezea sadaka, itakuwa mraba, kila upande mita 2. Mjengo wa kona za sehemu hii ya juu zitainuka kuliko sehemu nyingine.
16 Sehemu ya juu ya madhabahu itakuwa mraba, mita 6 kila upande.