7 naye akaniambia, “Wewe mtu! Hapa ndipo mahali pa kiti changu cha enzi, mahali niwekapo nyayo za miguu yangu. Nitakaa miongoni mwa watu wa Israeli milele. Na Waisraeli hawatalitia unajisi jina langu, wao wenyewe, wala wafalme wao kwa kuziabudu sanamu au kuzika maiti za wafalme wao mahali hapa.
8 Wafalme wao walijenga vizingiti na miimo ya ikulu zao karibu na vizingiti vya nguzo za hekalu langu, hivyo kati yangu na wao ulikuwa ni ukuta tu. Walilitia unajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyotenda, ndiyo maana nimewaangamiza kwa hasira yangu.
9 Sasa na waache kuziabudu sanamu na waziondoe maiti za wafalme wao mbali nami, nami nitakaa miongoni mwao milele.
10 “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda.
11 Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake.
12 Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”
13 Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25.