10 Mtawala ataingia ndani watu wanapoingia, na atatoka wanapotoka.
11 Wakati wa siku za sikukuu na siku zilizopangwa, sadaka za nafaka zitakuwa lita kumi na saba zikiandamana na kila fahali au kondoo dume, na chochote ambacho anayeabudu anaweza kutoa kwa kila mwanakondoo. Kwa kila sadaka ya nafaka atatoa lita tatu za mafuta.
12 Mtawala anapotaka kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kwa hiari, iwe sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, watamfungulia lango la ukumbi wa ndani unaoelekea mashariki. Atatoa sadaka kama anavyofanya siku ya sabato, na anapotoka, lango lifungwe nyuma yake.
13 “Kila siku asubuhi mtamtolea Mwenyezi-Mungu mwanakondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, ambaye atateketezwa mzima.
14 Pia kila siku, sadaka ya kilo mbili za unga itatolewa asubuhi pamoja na lita moja ya mafuta ya zeituni yakichanganywa na unga. Ni lazima kufuata sheria za sadaka hii kwa Mwenyezi-Mungu milele.
15 Mwanakondoo, unga na mafuta ni lazima vitolewe kila siku asubuhi kwa Mwenyezi-Mungu milele.
16 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ikiwa mtawala anampa mmojawapo wa wanawe zawadi ya ardhi, zawadi hiyo itakuwa mali ya huyo kijana milele kama sehemu ya jamaa yake.