12 Kisha ukingoni mwa mto huo kutaota kila namna ya miti itoayo chakula. Majani yake hayatanyauka wala miti hiyo haitaacha kuzaa matunda. Itazaa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu inapata maji yanayotiririka kutoka maskani ya Mungu. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatatumika kuponya magonjwa.”
13 Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Hii ndiyo mipaka ya nchi mtakayoyagawia makabila kumi na mawili ya Israeli. Lakini kabila la Yosefu lipewe maradufu.
14 Nyote mtagawana sawa. Niliapa kuwa nitawapa wazee wenu nchi hii, nayo itakuwa mali yenu.
15 Upande wa kaskazini mpaka utapita kutoka Bahari ya Mediteranea, kuelekea mji wa Hethloni, hadi mahali pa kuingia Hamathi na kuendelea hadi Zedadi.
16 Kutoka hapo utaendelea hadi Berotha na Sibraimu (ulio kati ya Damasko na Hamathi), hadi mji wa Haser-hatikoni ulio mpakani mwa Haurani.
17 Hivyo mpaka utakwenda kutoka bahari ya Mediteranea kuelekea mashariki hadi mji wa Hasar-enoni ukipakana na maeneo ya Damasko na Hamathi kwa upande wa kaskazini.
18 Upande wa mashariki, mpaka utakuwa mto wa Yordani unaoelekea kati ya Haurani na Damasko, Gileadi na nchi ya Israeli. Pia mpaka utapitia upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi hadi Tamari.