12 Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, umeona wanayotenda wazee wa Waisraeli gizani, kila mtu katika chumba chake cha sanamu. Wanadai ati Mwenyezi-Mungu hatuoni. Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi.”
13 Tena akaniambia, “Bado utaona machukizo makubwa zaidi wanayotenda.”
14 Kisha akanichukua mpaka lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko kulikuwa na wanawake wameketi wakimwombolezea Tamuzi.
15 Mungu akaniambia: “Wewe mtu, umeyaona hayo? Bado utaona machukizo mengine makubwa kuliko hayo.”
16 Kisha akanipeleka mpaka ua wa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko mlangoni mwa hekalu, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano, wakilipa kisogo hekalu, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki. Walikuwa wanaabudu jua wakielekea upande wa mashariki.
17 Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je umeyaona mambo hayo? Hata hivyo, watu wa Yuda wanaona machukizo hayo kuwa ni kidogo. Wanaijaza nchi dhuluma na kuzidi kunikasirisha. Angalia jinsi wamekaa hapo, wananiudhi kupita kiasi.
18 Kwa sababu ya mambo hayo watasikia uzito wa ghadhabu yangu. Sitamwacha hata mmoja aponyoke wala sitamwonea huruma mtu yeyote. Hata wakinililia kwa sauti kubwa mimi sitawasikiliza.”