12 Siku ya tatu na ya saba mtu huyo atajiosha kwa yale maji ya utakaso, naye atakuwa safi. Lakini akiacha kujitakasa katika siku ya tatu na ya saba, mtu huyo atabaki kuwa najisi.
13 Agusaye maiti, yaani mwili wa mtu aliyekufa, asipojitakasa, analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu, naye atatengwa na wana wa Israeli. Mtu huyo atabaki najisi kwa sababu hakunyunyiziwa yale maji ya utakaso.
14 “Na hii ndiyo sheria ya kufuatwa kama mtu akifia hemani: Kila mtu atakayeingia ndani ya hema hilo, au aliye ndani ya hema hilo, atakuwa najisi kwa siku saba.
15 Kila chombo kilicho wazi ambacho hakina kifuniko juu yake kitakuwa najisi.
16 Mtu yeyote akigusa mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida nje ya nyumba, au akigusa mfupa wa mtu au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.
17 “Kwa ajili ya wale waliojitia najisi watachukua majivu ya sadaka ya kuondoa dhambi iliyoteketezwa, majivu hayo yatachanganywa na maji ya mtoni katika chungu.
18 Mtu aliye safi atachukua husopo, halafu ataichovya katika maji hayo, kisha atainyunyizia hema, vyombo vyote vilivyomo ndani ya hema na watu waliokuwamo ndani. Atamnyunyizia pia mtu aliyegusa mfupa wa mtu, au mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida, au aliyegusa kaburi.