1 Vifuatavyo ni vituo ambavyo Waisraeli walipiga kambi walipotoka Misri wakiwa katika makundi ya makabila yao chini ya uongozi wa Mose na Aroni.
2 Mose aliandika jina la kila mahali walipopiga kambi, kituo baada ya kituo, kwa agizo la Mwenyezi-Mungu.
3 Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi mnamo siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, siku moja baada ya Pasaka ya kwanza. Waliondoka kwa uhodari mkubwa mbele ya Wamisri wote,
4 ambao walikuwa wanawazika wazaliwa wao wa kwanza wa kiume aliowaua Mwenyezi-Mungu; kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa ameiadhibu hata miungu yao.
5 Basi, Waisraeli waliondoka Ramesesi, wakapiga kambi yao huko Sukothi.
6 Kutoka Sukothi, walipiga kambi yao huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa.
7 Kutoka Ethamu, waligeuka na kurudi hadi Pi-hahirothi, mashariki ya Baal-sefoni, wakapiga kambi yao karibu na Migdoli.
8 Waliondoka Pi-hahirothi, wakapita bahari ya Shamu mpaka jangwa la Ethamu; walisafiri jangwani mwendo wa siku tatu, wakapiga kambi yao Mara.
9 Kutoka Mara, walisafiri hadi Elimu; huko Elimu kulikuwa na chemchemi kumi na mbili za maji na mitende sabini, wakapiga kambi yao mahali hapo.
10 Walisafiri kutoka Elimu, wakapiga kambi yao karibu na bahari ya Shamu.
11 Kutoka Bahari ya Shamu walipiga kambi yao katika jangwa la Sini.
12 Kutoka jangwa la Sini, walipiga kambi yao Dofka.
13 Kutoka Dofka walipiga kambi yao huko Alushi.
14 Kutoka Alushi walipiga kambi yao huko Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya kunywa.
15 Waliondoka Refidimu wakapiga kambi yao katika jangwa la Sinai.
16 Kutoka Sinai walipiga kambi yao huko Kibroth-hataava.
17 Kutoka Kibroth-hataava, walipiga kambi yao huko Haserothi.
18 Kutoka Haserothi, walipiga kambi yao huko Rithma.
19 Kutoka Rithma, walipiga kambi yao huko Rimon-perezi.
20 Kutoka Rimon-perezi, walipiga kambi yao huko Libna.
21 Kutoka Libna walipiga kambi yao Risa.
22 Waliondoka Risa, wakapiga kambi yao huko Kehelatha.
23 Kutoka Kehelatha, walipiga kambi yao kwenye Mlima Sheferi.
24 Kutoka Mlima Sheferi walipiga kambi yao huko Harada.
25 Kutoka Harada, walipiga kambi yao huko Makelothi.
26 Kutoka Makelothi, walipiga kambi yao huko Tahathi.
27 Kutoka Tahathi walipiga kambi yao Tera.
28 Kutoka Tera walipiga kambi yao Mithka.
29 Kutoka Mithka, walipiga kambi yao Hashmona.
30 Kutoka Hashmona, walipiga kambi yao Moserothi.
31 Kutoka Moserothi, walipiga kambi yao Bene-yaakani.
32 Kutoka Bene-yaakani, walipiga kambi yao Hor-hagidgadi.
33 Kutoka Hor-hagidgadi, walipiga kambi yao Yot-batha.
34 Kutoka Yot-batha, walipiga kambi yao Abrona.
35 Kutoka Abrona, walipiga kambi yao Esion-geberi.
36 Waliondoka Esion-geberi, wakasafiri na kupiga kambi yao katika jangwa la Sini, (yaani Kadeshi).
37 Kutoka Kadeshi, walipiga kambi yao mlimani Hori, mpakani mwa nchi ya Edomu.
38 Kwa agizo la Mwenyezi-Mungu kuhani Aroni alipanda juu ya Mlima Hori, na huko, akafariki mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tano, mwaka wa arubaini tangu Waisraeli walipotoka nchini Misri.
39 Aroni alikuwa na umri wa miaka 123 alipofariki juu ya Mlima Hori.
40 Mfalme wa Aradi, Mkanaani, aliyekaa Negebu katika nchi ya Kanaani, alipata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja.
41 Kutoka Mlima Hori, Waisraeli walipiga kambi yao Salmona.
42 Kutoka Salmona, walipiga kambi yao Punoni.
43 Kutoka Punoni, walipiga kambi yao Obothi.
44 Kutoka Obothi, walipiga kambi yao Iye-abarimu, katika eneo la Moabu.
45 Kutoka Iye-abarimu, walipiga kambi yao Dibon-gadi.
46 Kutoka Dibon-gadi, walisafiri na kupiga kambi yao Almon-diblathaimu.
47 Kutoka Almon-diblathaimu, walisafiri na kupiga kambi yao katika milima ya Abarimu, karibu na Mlima Nebo.
48 Kutoka milima ya Abarimu, walisafiri na kupiga kambi yao katika tambarare za Moabu ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko.
49 Walipiga kambi hiyo karibu na mto Yordani kati ya Beth-yeshimothi na bonde la Abel-shitimu kwenye tambarare za Moabu.
50 Katika tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko, Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
51 “Waambie Waisraeli kwamba mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ya Kanaani,
52 wafukuzeni wenyeji wote wa nchi hiyo mbele yenu. Mtaziharibu sanamu zao zote za mawe na za kusubu na kupabomoa kila mahali pao pa juu pa ibada.
53 Mtaichukua nchi hiyo na kukaa humo kwa sababu nimewapeni muimiliki.
54 Mtaigawanya nchi hiyo kwa kura kufuata familia zenu; eneo kubwa kwa kabila kubwa na eneo dogo kwa kabila dogo.
55 Lakini kama msipowafukuza wenyeji wa nchi hiyo kwanza, basi wale mtakaowaacha watakuwa kama vibanzi machoni mwenu au miiba kila upande, na watawasumbua.
56 Nami nitawafanyeni nyinyi kama nilivyokusudia kuwafanya wao.”