Hesabu 27 BHN

Haki ya kurithi kwa wanawake

1 Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza walikuwa binti zake Selofehadi. Naye Selofehadi alikuwa mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwanawe Yosefu.

2 Basi, hao binti wanne walimwendea Mose, wakasimama mbele yake na kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli, kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasema,

3 “Baba yetu alifia jangwani nyikani na bila mtoto yeyote wa kiume.

4 Yeye hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora waliokusanyika dhidi ya Mwenyezi-Mungu, bali alikufa kutokana na dhambi yake mwenyewe. Kwa nini basi jina la baba yetu lifutwe katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume? Tupe urithi pamoja na ndugu zake baba yetu.”

5 Mose akaleta lalamiko lao mbele ya Mwenyezi-Mungu.

6 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

7 “Wanachosema binti za Selofehadi ni kweli; wape urithi pamoja na ndugu za baba yao, wachukue urithi wake.

8 Kisha waambie Waisraeli kwamba mtu yeyote akifa bila kuacha mtoto wa kiume, urithi wake atapewa binti yake.

9 Ikiwa hana binti, basi urithi huo watapewa ndugu zake wa kiume.

10 Na ikiwa hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utawaendea baba zake, wakubwa na wadogo.

11 Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.”

Yoshua ateuliwa kuwaongoza Waisraeli

12 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli.

13 Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki,

14 kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini).

15 Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu,

16 “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote, nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii,

17 ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.”

18 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono,

19 na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo.

20 Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii.

21 Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.”

22 Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli.

23 Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31 32 33 34 35 36