1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2 “Tengeneza tarumbeta mbili kwa fedha iliyofuliwa. Utazitumia tarumbeta hizo wakati wa kuwaita watu na wakati wa kuvunja kambi.
3 Tarumbeta zote mbili zikipigwa pamoja, watu wote watakusanyika karibu nawe mbele ya lango la hema la mkutano.
4 Lakini kama ikipigwa tarumbeta moja tu, basi ni viongozi tu wa makabila ya Israeli watakaokusanyika karibu nawe.
5 Ishara hiyo ikitolewa kwa kupiga tarumbeta, wakazi wa kambi za mashariki wataanza safari.
6 Ishara hiyo ikipigwa mara ya pili, wale wa kambi za upande wa kusini wataanza kuondoka. Ishara hiyo ya tarumbeta itatolewa kila wakati wa kuanza safari.
7 Lakini wakati wa kuwaita watu wakusanyike pamoja, tarumbeta zitapigwa kwa njia ya kawaida.
8 Wazawa wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga tarumbeta hizo. Utaratibu huo utafuatwa daima katika vizazi vyenu vyote.
9 “Wakati wa vita nchini mwenu dhidi ya adui wanaowashambulia, mtatoa ishara ya vita kwa kupiga tarumbeta hizi ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu apate kuwakumbuka na kuwaokoa na adui zenu.
10 Hali kadhalika katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyinginezo, mtazipiga tarumbeta hizi wakati mnapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na tambiko za sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbukeni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”
11 Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa,
12 nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani.
13 Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose.
14 Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu.
15 Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari.
16 Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni.
17 Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka.
18 Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Reubeni, walifuata kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.
19 Shelumieli mwana wa Suri-shadai, aliliongoza kabila la Simeoni.
20 Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliliongoza kabila la Gadi.
21 Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohathi, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipowasili, hema lilikuwa limekwisha simikwa.
22 Baada ya hao, walifuata watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Efraimu, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elishama mwana wa Amihudi.
23 Gamalieli mwana wa Pedasuri aliliongoza kabila la Manase,
24 naye Abidani mwana wa Gideoni, aliliongoza kabila la Benyamini.
25 Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya vikosi vyote, walisafiri, kundi moja baada ya jingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai.
26 Pagieli, mwana wa Okrani, aliliongoza kabila la Asheri.
27 Naye Ahira mwana wa Enani, aliliongoza kabila la Naftali.
28 Huu basi, ndio utaratibu walioufuata Waisraeli kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena.
29 Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.”
30 Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.”
31 Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu.
32 Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.”
33 Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi.
34 Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana.
35 Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.”
36 Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.”