1 Jumuiya yote ya Waisraeli ikaangua kilio kikubwa, watu wakalia usiku ule.
2 Waliwalalamikia Mose na Aroni wakisema, “Afadhali tungefia Misri! Afadhali tungefia papa hapa jangwani!
3 Kwa nini Mwenyezi-Mungu anatupeleka katika nchi hiyo? Tutauawa vitani, na wake zetu na watoto wetu watachukuliwa mateka! Si afadhali turudi Misri?”
4 Basi wakaanza kuambiana, “Na tuchague kiongozi, turudi Misri.”
5 Hapo, Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli.
6 Yoshua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ambao walikuwa miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi, wakazirarua nguo zao
7 na kuiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Nchi tuliyokwenda kuipeleleza ni nzuri kupita kiasi.
8 Ikiwa Mwenyezi-Mungu amependezwa nasi, atatupeleka huko na kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali.
9 Mradi tu msimwasi Mwenyezi-Mungu, wala msiwaogope wenyeji wa nchi hiyo. Maana wao ni mboga tu kwetu; kinga yao imekwisha ondolewa kwao, naye Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi; msiwaogope!”
10 Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote.
11 Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Watu hawa watanidharau mpaka lini? Na, mpaka lini wataendelea kutoniamini, hata pamoja na miujiza yote niliyotenda kati yao?
12 Nitawapiga kwa maradhi mabaya na kuwatupilia mbali; lakini, kutokana nawe, nitaunda taifa lingine kubwa, lenye nguvu kuliko wao.”
13 Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Uliwatoa watu hawa nchini Misri kwa nguvu yako. Wamisri watakaposikia kwamba umewatenda hivyo watu wako,
14 watawapasha habari wakazi wa nchi hii. Maana watu hawa wamekwisha pata habari kwamba wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi; maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu, unaonekana waziwazi wingu lako linaposimama juu yetu, na kwamba wewe hututangulia mchana kwa nguzo ya wingu na usiku kwa nguzo ya moto.
15 Sasa basi, ukiwaua watu wako wote kwa mara moja, mataifa ambayo yamekwisha sikia sifa zako yatasema,
16 ‘Mwenyezi-Mungu aliwaua watu wake jangwani kwa sababu alishindwa kuwapeleka katika nchi aliyoahidi kuwapa.’
17 Basi, sasa nakusihi, ee Mwenyezi-Mungu, utuoneshe uwezo wako kwa kufanya kama ulivyotuahidi uliposema,
18 ‘Mimi Mwenyezi-Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwenye fadhili nyingi, na ni mwenye kusamehe uovu na makosa. Lakini kwa vyovyote vile sitakosa kuwaadhibu watoto na wajukuu hadi kizazi cha tatu na cha nne kwa dhambi za wazazi wao.’
19 Nakusihi uwasamehe watu hawa dhambi zao, kadiri ya fadhili zako nyingi kama vile ulivyowasamehe tangu watoke Misri hadi sasa.”
20 Mwenyezi-Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba.
21 Lakini kwa kweli, kama niishivyo na kadiri dunia itakavyojaa utukufu wangu,
22 hakuna hata mmoja wao ambaye amewahi kuuona utukufu wangu na miujiza yangu niliyoifanya Misri na jangwani kisha akazidi kunijaribu mara hizi zote bila ya kutii sauti yangu,
23 ataiona nchi ile niliyoapa kuwapatia babu zao; kadhalika hata wale wanaonidharau pia hawataiona.
24 Bali kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ni tofauti, na amenitii kikamilifu, nitamfikisha kwenye nchi hiyo aliyoingia na wazawa wake wataimiliki.
25 Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanakaa katika mabonde ya nchi hiyo, kesho geukeni nyuma mwende jangwani kuelekea bahari ya Shamu.”
26 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwuliza Mose na Aroni,
27 “Kundi hili la watu waovu litaendelea kuninungunikia mpaka lini? Nimechoka na haya manunguniko ya Waisraeli juu yangu!
28 Sasa wajibu hivi: Kama niishivyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitawatendeeni yaleyale niliyosikia mkiyasema:
29 Mtakufa na miili yenu itatupwa humuhumu jangwani, kwa sababu mmenungunika dhidi yangu, hakuna hata mmoja wenu mwenye umri wa kuanzia miaka ishirini na zaidi,
30 atakayeingia katika nchi hiyo ambayo niliapa kuwapa iwe yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.
31 Nyinyi mlisema kuwa watoto wenu watatekwa nyara, lakini mimi nitawafikisha watoto wenu kwenye nchi mliyoidharau, ili waijue na iwe makao yao.
32 Lakini nyinyi, mtafia humuhumu jangwani.
33 Watoto wenu watatangatanga na kutaabika humu jangwani kwa muda wa miaka arubaini kwa ajili ya ukosefu wenu wa imani mpaka mtu wenu wa mwisho atakapofia jangwani.
34 Kutokana na makosa yenu, mtataabika kwa muda wa miaka arubaini, sawa na zile siku arubaini mlizopeleleza ile nchi, mwaka mmoja kwa kila siku moja; mtatambua kwamba mimi nimechukizwa.
35 Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema: Hakika nitawatenda hivyo nyinyi nyote mliokusanyika hapa kunipinga. Wote wataishia humuhumu jangwani na ni humu watakamofia.”
36 Wale watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza ile nchi waliorudi na kusababisha watu wamnungunikie Mwenyezi-Mungu kwa kuleta taarifa mbaya dhidi ya nchi,
37 watu hao waliotoa taarifa ya uovu kuhusu hiyo nchi, walikufa kwa pigo mbele ya Mwenyezi-Mungu.
38 Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, walibaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.
39 Naye Mose aliwaambia Waisraeli wote nao walilia kwa uchungu mwingi.
40 Kesho yake, waliamka alfajiri na mapema wakaenda sehemu za milimani, wakisema, “Sasa tuko tayari kabisa kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alituahidi. Tunakiri kwamba tulitenda dhambi.”
41 Lakini Mose akasema, “Sasa mbona mnavunja agizo la Mwenyezi-Mungu? Hivyo hamtafaulu!
42 Msiende huko milimani msije mkapigwa bure na adui zenu, maana, Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja nanyi.
43 Mkiwakabili Waamaleki na Wakanaani, mtafia vitani; kwa kuwa mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu, yeye hatakuwa pamoja nanyi.”
44 Hata hivyo, wao walisisitiza kwenda juu milimani, ingawa sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wala Mose hakuondoka kambini.
45 Ndipo Waamaleki na Wakanaani, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo ya milima, wakashuka, wakawashambulia na kuwashinda. Wakawafukuza mpaka mji wa Horma.