1 Viongozi wa jamaa katika ukoo wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, mwana wa Yosefu, walikwenda kuzungumza na Mose na viongozi wengine wa koo za Waisraeli.
2 Wakasema, “Bwana wetu, Mwenyezi-Mungu alikuamuru kuwagawia watu wa Israeli nchi kwa kura, kuwa urithi wao; alikuamuru pia uwape binti za Selofehadi ndugu yetu urithi wa baba yao.
3 Lakini wao wakiolewa na Waisraeli wa makabila mengine, urithi wao utatoka kwetu na kuwaendea watu wa kabila watakamoolewa; kwa hiyo urithi wetu sisi utapungua.
4 Katika sikukuu ya ukumbusho urithi wao utahesabiwa pamoja na ule wa kabila watakamoolewa na hivyo kabila letu halitapata urithi huo tena.”
5 Basi, Mose akawapa Waisraeli agizo lifuatalo kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, akawaambia, “Watu wa ukoo wa kabila la Yosefu, wamesema ukweli.
6 Na hivi ndivyo anavyoamuru Mwenyezi-Mungu kuhusu binti za Selofehadi; wako huru kuolewa na mtu yeyote wampendaye, lakini waolewe katika kabila lao,
7 ili urithi wa Waisraeli usihamishiwe kwa kabila lingine; kila Mwisraeli atazingatia urithi wa kabila lake.
8 Mwanamke yeyote mwenye urithi katika kabila mojawapo la Israeli ni lazima aolewe na mtu wa kabila lake, ili kila Mwisraeli achukue urithi wa babu zake.
9 Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaohamishwa kutoka kabila moja hadi jingine. Kila kabila la Waisraeli litashikilia urithi wake.”
10 Binti za Selofehadi walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
11 Wote: Mala, Tirza, Hogla, Milka na Noa wakaolewa na binamu zao.
12 Waliolewa katika jamaa za ukoo wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika kabila la baba yao.
13 Hizo ndizo amri na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Mose katika tambarare za Moabu, ngambo ya Mto Yordani karibu na mji wa Yeriko.