1 Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa kisha uniletee fahali saba na kondoo madume saba.”
2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema. Basi, wakatoa juu ya kila madhabahu kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja.
3 Halafu Balaamu akamwambia Balaki, “Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami niende. Labda Mwenyezi-Mungu atakutana nami. Chochote atakachonionesha nitakuja kukuambia.” Basi, Balaamu akaenda peke yake juu ya kilele cha mlima.
4 Mungu akakutana naye. Balaamu akamwambia, “Nimetayarisha madhabahu saba na kutoa kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.”
5 Mwenyezi-Mungu akampa Balaamu maneno atakayosema na kumwambia arudi kwa Balaki.
6 Balaamu akarudi, akamkuta Balaki amesimama palepale karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, pamoja na maofisa wote wa Moabu.
7 Balaamu akamtolea Balaki kauli yake, akasema,“Balaki amenileta hapa kutoka Aramu,naam, mfalme wa Moabu amenileta kutoka milima ya mashariki.‘Njoo uwalaani watu wa Yakobo kwa ajili yangu,naam, njoo uwalaumu Waisraeli!’
8 Nitamlaanije mtu ambaye Mungu hakumlaani?Nitawalaumuje watu ambao Mwenyezi-Mungu hakuwalaumu?
9 Kutoka vilele vya majabali nawaona;kutoka juu ya milima nawachungulia.Hilo taifa likaalo peke yake,lisilojiona kuwa sawa na mataifa mengine.
10 Nani awezaye kuwahesabu wingi wa watu wa Yakobo,au kukisia umati wa Waisraeli?Nife kifo cha waadilifu,mwisho wangu na uwe kama wao.”
11 Hapo, Balaki akamwambia Balaamu, “Umenifanyia nini? Nimekuleta hapa uwalaani adui zangu, lakini badala yake umewabariki!”
12 Balaamu akamwambia Balaki, “Sina budi kusema maneno aliyonipa Mwenyezi-Mungu.”
13 Baadaye, Balaki akamwambia Balaamu, “Twende mahali pengine ambapo utaweza kuwaona; hata hivyo utaona tu sehemu yao, hutaweza kuwaona wote. Kisha uwalaani kutoka huko kwa niaba yangu.”
14 Basi, Balaki akamchukua Balaamu kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Hapo akajenga madhabahu saba na kutoa juu ya kila madhabahu kafara ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.
15 Balaamu akamwambia Balaki, “Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami niende kule ngambo kukutana na Mwenyezi-Mungu.”
16 Mwenyezi-Mungu akakutana na Balaamu, akampa maneno atakayosema, na kumwambia arudi kwa Balaki.
17 Basi, Balaamu akarudi, akamkuta Balaki amesimama karibu na sadaka ya kuteketezwa pamoja na maofisa wote wa Moabu. Balaki akamwuliza, “Mwenyezi-Mungu amekuambia nini?”
18 Hapo, Balaamu akamtolea Balaki kauli yake:“Inuka, Balaki, usikie,nisikilize ewe mwana wa Sipori.
19 Mungu si mtu, aseme uongo,wala si binadamu, abadili nia yake!Je, ataahidi kitu na asikifanye,au kusema kitu asikitimize?
20 Tazama, nimepewa amri ya kubariki,naye amebariki wala siwezi kuitangua.
21 Mwenyezi-Mungu hajaona ubaya kwa wana wa Yakobo,wala udhia kwa hao wana wa Israeli.Mwenyezi-Mungu Mungu wao yuko pamoja nao,Yeye husifiwa kwa vifijo miongoni mwao,yeye huzipokea sifa zao za kifalme.
22 Mungu aliyewachukua kutoka Misri,huwapigania kwa nguvu kama za nyati.
23 Hakika ulozi hauwezi kuwapinga watu wa Yakobo,wala uchawi dhidi ya watu wa Israeli.Sasa kuhusu Israeli, watu watasema,‘Tazameni maajabu aliyotenda Mungu!’
24 Tazama! Waisraeli wameinuka kama simba jike,wanasimama kama simba dume.Ni kama simba asiyelala mpaka amalize mawindo yake,na kunywa damu ya mawindo.”
25 Ndipo Balaki akamwambia Balaamu, “Basi, usiwalaani wala usiwabariki kabisa!”
26 Lakini Balaamu akamjibu Balaki, “Je, sikukuambia kwamba anachosema Mwenyezi-Mungu ndicho ninachopaswa kufanya?”
27 Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo; nitakupeleka mahali pengine. Labda Mungu atakubali uwalaani watu hao kutoka huko kwa ajili yangu.”
28 Basi, Balaki akamchukua Balaamu mpaka kwenye kilele cha Mlima Peori, ambapo mtu akisimama anaona jangwani.
29 Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa, unitayarishie fahali saba na kondoo madume saba.”
30 Balaki akafanya kama alivyoambiwa na Balaamu, kisha akatoa juu ya kila madhabahu kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja.