1 Mfalme mmoja Mkanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu alipopata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, alikwenda kuwashambulia, akawateka baadhi yao.
2 Hapo, Waisraeli wakamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri wakisema: “Kama utawatia watu hawa mikononi mwetu, basi tutaiangamiza kabisa miji yao.”
3 Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma.
4 Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo.
5 Basi, wakaanza kumnungunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.”
6 Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa.
7 Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnungunikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu.
8 Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.”
9 Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona.
10 Waisraeli waliendelea na safari yao, wakapiga kambi huko Obothi.
11 Kutoka huko walisafiri mpaka Iye-abarimu, katika jangwa upande wa mashariki, mwa Moabu.
12 Kutoka huko walisafiri wakapiga kambi yao katika bonde la Zeredi.
13 Kutoka huko walisafiri, wakapiga kambi kaskazini ya mto Arnoni, ambao hutiririka kutoka katika nchi ya Waamori na kupitia jangwani. Mto Arnoni ulikuwa mpaka kati ya Wamoabu na Waamori.
14 Kwa sababu hiyo, imeandikwa katika kitabu cha vita vya Mwenyezi-Mungu:“Mji wa Wahebu nchini Sufa,na mabonde ya Arnoni,
15 na mteremko wa mabondeunaofika hadi mji wa Ari,na kuelekea mpakani mwa Moabu!”
16 Kutoka huko Waisraeli walisafiri mpaka Beeri; yaani kisima ambapo Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wakusanyeni watu pamoja, nami nitawapa maji.”
17 Hapo Waisraeli waliimba wimbo huu:“Bubujika maji ee kisima! – Kiimbieni!
18 Kisima kilichochimbwa na wakuukilichochimbwa sana na wenye cheo,kwa fimbo zao za enzi na bakora.”Kutoka jangwani walisafiri mpaka Matana,
19 kutoka Matana mpaka Nahalieli, kutoka Nahalieli mpaka Bamothi,
20 na kutoka Bamothi mpaka kwenye bonde linaloingia nchi ya Moabu, kwenye kilele cha Mlima Pisga, kielekeacho chini jangwani.
21 Waisraeli walimpelekea mfalme Sihoni wa Waamori, ujumbe huu:
22 “Turuhusu tupite katika nchi yako; hatutakwenda pembeni na kuingia mashambani au katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visima vyenu; tutapita moja kwa moja katika barabara kuu ya mfalme mpaka tumeondoka nchini mwako.”
23 Lakini Sihoni hakuwaruhusu watu wa Israeli wapite katika nchi yake. Aliwakusanya watu wake, akaenda Yahasa Jangwani kuwashambulia Waisraeli.
24 Lakini Waisraeli walimuua, wakaitwaa nchi yake tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki, yaani hadi mpaka wa nchi ya Waamoni ambao ulikuwa unalindwa sana.
25 Waisraeli waliiteka miji hii yote nao wakaishi katika miji ya Waamori katika Heshboni na vitongoji vyake.
26 Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye hapo awali alikuwa amepigana na mfalme wa Moabu na kuiteka nchi yake yote mpaka mto Arnoni.
27 Ndiyo maana washairi wetu huimba:“Njoni Heshboni na kujenga.Mji wa Sihoni na ujengwe na kuimarishwa.
28 Maana moto ulitoka Heshboni,miali ya moto ilitoka mjini kwa Sihoni,uliuteketeza mji wa Ari wa Moabu,ukaiangamiza milima ya mto Arnoni.
29 Ole wenu watu wa Moabu!Mmeangamizwa, enyi watu wa mungu Kemoshi!Umewafanya watoto wenu wa kiume kuwa wakimbizi,binti zako umewaacha wachukuliwe matekampaka kwa Sihoni, mfalme wa Amori.
30 Lakini sasa wazawa wao wameangamizwa,kutoka Heshboni mpaka Diboni,kutoka Nashimu mpaka Nofa, karibu na Medeba.”
31 Basi, Waisraeli wakakaa katika nchi ya Waamori.
32 Kisha Mose alituma watu wapeleleze mji wa Yazeri; wakauteka pamoja na vitongoji vyake, wakawafukuza Waamori waliokaa humo.
33 Waisraeli waligeuka wakafuata njia iendayo Bashani. Mfalme Ogu wa Bashani akatoka na jeshi lake kuwashambulia huko Edrei.
34 Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake wote na nchi yake yote. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa anakaa Heshboni.”
35 Basi, Waisraeli wakamuua Ogu, wanawe na watu wake wote, bila kumwacha hata mtu mmoja, kisha wakaitwaa nchi yake.