6 Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya mwezi mpya na sadaka yake ya nafaka, na sadaka ya kila siku ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji kama inavyotakiwa kuwa harufu nzuri ipendezayo, ni sadaka kwa Mwenyezi-Mungu iliyoteketezwa kwa moto.
7 “Siku ya kumi ya mwezi wa saba mtafanya mkutano mtakatifu. Siku hiyo ni lazima mfunge na msifanye kazi.
8 Mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, wanakondoo saba wa mwaka mmoja. Wote wasiwe na dosari.
9 Licha ya vitu hivi mtatoa sadaka ya unga safi uliochanganywa na mafuta kilo tatu pamoja na huyo fahali, kilo mbili pamoja na yule kondoo dume,
10 na kilo moja kwa kila mwanakondoo.
11 Mtatoa pia beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi licha ya sadaka ya kufanyiwa upatanisho, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji.
12 “Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtafanya mkutano mtakatifu. Hamtafanya kazi siku hiyo. Mtaadhimisha sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu kwa siku saba.