12 Wote hawataiona, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, maana wao wamenitii kikamilifu.
13 Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira dhidi ya Waisraeli, akawafanya watangetange jangwani kwa muda wa miaka arubaini; kizazi kizima kilichokuwa kimefanya maovu mbele yake kikafariki.
14 Na sasa, enyi kizazi cha wenye dhambi, mmezuka mahali pa wazee wenu, kuongeza tena hasira kali ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Waisraeli.
15 Kama nyinyi mkikataa kumfuata, yeye atawaacheni tena jangwani, nanyi mtasababisha watu hawa wote waangamie.”
16 Basi, wakamwendea Mose, wakamwambia, “Kwanza turuhusu tuwajengee kondoo wetu mazizi, na watoto wetu miji hapa.
17 Lakini sisi wenyewe tutachukua silaha zetu tayari kwenda vitani pamoja na ndugu zetu Waisraeli, na tutakuwa mstari wa mbele vitani hadi tuwafikishe mahali watakapokaa. Wakati huo watoto wetu watakaa kwenye miji yenye ngome, ili kujilinda na wenyeji wa nchi hii.
18 Hatutarudi nyumbani hadi hapo Waisraeli wengine wote watakapomiliki maeneo yao waliyogawiwa.