20 Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako,
21 Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe.
22 Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’
23 “Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu;
24 naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali;
25 kisha kuhani atachukua ile sadaka ya nafaka ya wivu mikononi mwa mwanamke huyo na kuitikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuipeleka madhabahuni.
26 Halafu, atatwaa konzi moja ya sadaka hiyo ya nafaka kwa ukumbusho na kuiteketeza madhabahuni. Hatimaye atamnywesha mwanamke maji hayo.