3 walimletea Mwenyezi-Mungu matoleo yao: Magari yaliyofunikwa sita na mafahali kumi na wawili, gari moja kwa kila viongozi wawili na fahali mmoja kwa kila kiongozi. Baada ya kuvitoa mbele ya hema takatifu,
4 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
5 “Pokea matoleo haya ili yatumiwe katika huduma itakayofanywa kwa ajili ya hema la mkutano, uwape Walawi, kila mmoja kwa kadiri ya kazi yake.”
6 Basi, Mose akachukua magari na mafahali akawapa Walawi.
7 Wagershoni wakapewa magari mawili na mafahali wanne, kwa kadiri ya huduma yao,
8 na Wamerari wakapewa magari manne na mafahali wanane, kuwasaidia katika kazi zao zote chini ya uongozi wa Ithamari mwana wa kuhani Aroni.
9 Lakini Mose hakuwapa chochote Wakohathi kwa kuwa wao walikuwa na jukumu la kutunza vitu vitakatifu ambavyo vilipaswa kubebwa mabegani.