1 Kisha mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika jangwa la Sinai. Alimwambia:
2 “Waisraeli sharti waiadhimishe sikukuu ya Pasaka wakati uliopangwa.
3 Hii itakuwa siku ya kumi na nne ya mwezi huu; wakati wa jioni watafanya hivyo kufuatana na masharti na maagizo yake yote.”
4 Kwa hiyo, Mose akawaambia watu kwamba wanapaswa kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka.
5 Basi, wakaiadhimisha Pasaka jioni, siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, katika jangwa la Sinai. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.