1 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao. Mimi nimemfanya kuwa mkaidi na maofisa wake ili nipate kutenda ishara hizi miongoni mwao,
2 ili nyinyi mpate kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu, jinsi nilivyowadhihaki Wamisri kwa kuzifanya ishara hizo miongoni mwao. Hivyo mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
3 Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, anasema hivi, ‘Mpaka lini utakataa kujinyenyekesha mbele yangu? Waache watu wangu waondoke ili wapate kunitumikia.
4 Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako.
5 Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani.