16 Hapo Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka, akawaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu.
17 Kwa hiyo sasa ninawasihi mnisamehe dhambi yangu, mara hii moja tu, mkaniombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki.”
18 Basi, Mose akaondoka kwa Farao, akaenda kumwomba Mwenyezi-Mungu.
19 Naye Mwenyezi-Mungu akaleta upepo mkali toka magharibi, ukawainua wale nzige na kuwasukumia kwenye bahari ya Shamu. Hakuna hata nzige mmoja aliyebaki katika nchi nzima ya Misri.
20 Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachia Waisraeli waondoke.
21 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni ili giza nene litokee nchini Misri, giza nene ambalo mtu ataweza kulipapasa.”
22 Basi, Mose akanyosha mkono wake juu mbinguni, kukawa na giza nene kote nchini Misri kwa muda wa siku tatu.