1 Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
2 “Waambie Waisraeli warudi nyuma, wapige kambi mbele ya Pi-hahirothi, kati ya mji wa Migdoli na bahari ya Shamu, mbele ya Baal-sefoni. Mtapiga kambi mbele yake karibu na bahari.
3 Maana, Farao atafikiri, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga, nalo jangwa limewazuia wasiweze kutoka.’
4 Hapo mimi nitamfanya Farao kuwa mkaidi, naye atawafuatia. Nami nitajipatia utukufu kwa kumwangamiza yeye na jeshi lake. Hapo Wamisri watatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo.
5 Farao, mfalme wa Misri, aliposikia kwamba Waisraeli wamekimbia, yeye na maofisa wake walibadili fikira zao, wakasema, “Tumefanya nini kuwaachia Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?”
6 Basi, Farao akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake.
7 Alichukua magari yake bora ya vita 600 na magari yote mengine ya kivita ya Misri yakiongozwa na maofisa wa kijeshi.