12 Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.”
13 Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena.
14 Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.”
15 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
16 Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu.
17 Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake.
18 Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”