20 Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kingoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vingoma vyao wakicheza.
21 Miriamu akawaongoza kwa kuimba,“Mwimbieni Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.”
22 Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri. Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote.
23 Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara.
24 Basi, watu wote wakamlalamikia Mose wakisema, “Sasa tutakunywa nini?”
25 Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri.Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao,
26 akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya nyinyi.”