28 Hivyo Waisraeli daima watachukua sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu na kumpa Aroni na wanawe. Hiyo ni sadaka yao kwa Mwenyezi-Mungu.
29 “Baada ya kufa kwake Aroni, mavazi yake matakatifu yatakabidhiwa wazawa wake, nao watayavaa siku yao ya kupakwa mafuta na kuwekewa mikono.
30 Mwana wa Aroni atakayekuwa kuhani mahali pa baba yake atayavaa mavazi hayo siku saba katika hema la mkutano, ili kuhudumu katika mahali patakatifu.
31 “Utachukua nyama ya huyo kondoo wa kuwaweka wakfu na kuichemshia katika mahali patakatifu.
32 Kisha utawapa Aroni na wanawe, nao wataila mlangoni pa hema la mkutano pamoja na ile mikate iliyosalia kapuni.
33 Watavila vitu hivyo vilivyotumika kuwaweka wakfu na kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho, lakini mtu mwingine asiruhusiwe kuvila kwani ni vitakatifu.
34 Kama nyama yoyote au mikate hiyo itasalia mpaka asubuhi yake, basi utaiteketeza kwa moto; isiliwe maana ni kitu kitakatifu.