18 Samaki waliomo mtoni Nili watakufa, mto wote utanuka vibaya, na Wamisri watachukia kabisa kunywa maji yake.’”
19 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni aichukue fimbo yake na kuinyosha juu ya maji ya Misri, juu ya mito yote, mifereji, madimbwi na mabwawa yao yote, nayo yatakuwa damu. Kutakuwa na damu nchini kote, na hata katika vyombo vyote vya mbao na vya mawe.”
20 Mose na Aroni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Aroni aliinua fimbo yake juu mbele ya Farao na maofisa wake, akayapiga maji ya mto Nili, na maji yote mtoni yakageuka kuwa damu.
21 Samaki wakafa, mto ukanuka vibaya sana hata Wamisri wasiweze kunywa maji yake. Nchi nzima ikajaa damu.
22 Lakini wachawi wa Misri kwa kutumia uchawi wao wakafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo moyo wa Farao ukabaki kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni; ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.
23 Basi, Farao akarudi nyumbani kwake, na hata haya yaliyotokea hakuyajali.
24 Wamisri wote wakachimbachimba kandokando ya mto Nili ili wapate maji ya kunywa, kwani hawakuweza kunywa maji ya mto huo.