22 Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni, ili mvua ya mawe inyeshe kila mahali nchini Misri. Imnyeshee mtu, mnyama na kila mmea shambani.”
23 Basi, Mose alinyosha fimbo yake kuelekea mbinguni. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta mvua ya mawe na ngurumo; umeme ukaipiga nchi. Mwenyezi-Mungu alinyesha mvua ya mawe nchini Misri,
24 mvua kubwa ya mawe iliyoandamana na mfululizo wa umeme, ambayo hakuna mwananchi yeyote wa Misri aliyepata kamwe kushuhudia kabla.
25 Mvua hiyo ya mawe ilivunjavunja kila kitu katika mashamba na kila mahali nchini Misri: Wanyama na watu. Mawe ya mvua yakavunjavunja mimea yote na miti mashambani.
26 Jambo hilo lilifanyika kote nchini Misri isipokuwa tu sehemu ya Gosheni walimokaa Waisraeli; humo haikuwako mvua ya mawe.
27 Basi, Farao akaagiza Mose na Aroni waitwe, akawaambia, “Safari hii nimetenda dhambi. Mwenyezi-Mungu ana haki; mimi na watu wangu tumekosa.
28 Mwombeni Mwenyezi-Mungu kwani ngurumo hii na mvua ya mawe vimezidi. Mimi nitawaacheni mwondoke na wala hamtakaa tena zaidi.”