1 Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi-Mungu alimtokea, akamwambia, “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama.
2 Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.”
3 Hapo Abramu akasujudu. Naye Mungu akamwambia,
4 “Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba wa mataifa mengi.
5 Tangu sasa, hutaitwa tena Abramu, bali utaitwa Abrahamu, maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi.
6 Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana; kwako nitazusha mataifa mengi na wafalme.