15 Siku moja Labani alimwambia Yakobo, “Wewe ni jamaa yangu lakini hiyo haimaanishi kwamba utanitumikia bure. Niambie unataka ujira kiasi gani!”
16 Sasa, Labani alikuwa na binti wawili: Mkubwa aliitwa Lea, na mdogo aliitwa Raheli.
17 Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na wa kupendeza.
18 Yakobo alimpenda Raheli; kwa hiyo akamwambia Labani, “Nitakutumikia miaka saba ili unioze Raheli, binti yako mdogo.”
19 Labani akamwambia, “Afadhali nimwoze Raheli kwako wewe kuliko kumwoza mtu mwingine yeyote. Endelea kuishi nami.”
20 Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli.
21 Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.”