2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu.
3 Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu.
4 Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa.
5 Nina ng'ombe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’”
6 Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.”
7 Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia,
8 akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.”