8 Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao wakamtumikia kwa muda wa miaka minane.
9 Waisraeli wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawapelekea mtu wa kuwakomboa yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10 Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Othnieli, naye akawa mwamuzi wa Waisraeli. Othnieli alikwenda vitani naye Mwenyezi-Mungu akamtia Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwake.
11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Kisha Othnieli mwana wa Kenazi, akafariki.
12 Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akampa nguvu mfalme Egloni wa Moabu awashambulie Waisraeli, kwa sababu walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.
13 Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki, akaenda kupigana na Waisraeli, akawashinda. Akauteka Mji wa Mitende yaani Yeriko.
14 Waisraeli wakamtumikia Egloni mfalme wa Moabu, kwa muda wa miaka kumi na minane.