3 Ndugu za mama yake wakatangaza maneno haya kote Shekemu kwa niaba yake, na watu wote wa Shekemu wakaamua kumfuata maana alikuwa ndugu yao.
4 Wakampa vipande sabini vya fedha vilivyokuwa kwenye nyumba ya Baal-berithi ambavyo alivitumia kuwakodi watu wakorofi na watu ovyoovyo ili wamfuate.
5 Akafuatana nao kwenda Ofra kwa baba yake na huko akawaua ndugu zake wote sabini juu ya jiwe moja. Lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubabeli alinusurika, maana alijificha.
6 Wananchi wote wa Shekemu na Beth-milo wakakusanyika kwenye mwaloni ulio karibu na mnara huko Shekemu, wakamfanya Abimeleki kuwa mfalme wao.
7 Yothamu alipopata habari hizo, alikwenda kusimama juu ya mlima Gerizimu, akasema kwa sauti kubwa, “Nisikilizeni, enyi watu wa Shekemu kama mnataka Mungu awasikilize na nyinyi.
8 Siku moja, miti ilikwenda kujitafutia mfalme. Basi, ikauambia mzeituni, ‘Tawala juu yetu!’
9 Lakini mzeituni ukajibu, ‘Mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha mafuta ambayo huthaminiwa sana na miungu na wanadamu niende kujisumbua kuitawala miti?’