1 Mwenyezi-Mungu alimwita Mose na kuongea naye katika hema la mkutano, akamwambia,
2 “Waambie Waisraeli kwamba kama mtu anapenda kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mnyama, mnyama huyo atamchagua kutoka kundi lake la ng'ombe, kondoo au mbuzi.
3 “Kama sadaka anayotoa mtu ni ya kuteketezwa, atamchagua mnyama dume asiye na dosari kutoka kundi lake, atamtolea mbele ya mlango wa hema la mkutano ili apate fadhili ya Mwenyezi-Mungu;
4 ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo itakubaliwa kwa ajili ya kumfanyia huyo mtu upatanisho.
5 Kisha, atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani, wazawa wa Aroni, wataichukua damu na kuinyunyizia madhabahu mlangoni mwa hema la mkutano, pande zake zote.
6 Huyo mtu atamchuna huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kumkata vipandevipande.