7 Basi, nikawa mchungaji wa kondoo waliokuwa wanakwenda kuchinjwa, kwani niliajiriwa na wale waliofanya biashara ya kondoo. Nikachukua fimbo mbili: Moja nikaiita “Fadhili,” na nyingine nikaiita “Umoja,” nikaenda kuchunga kondoo.
8 Kwa muda wa mwezi mmoja, nikaua wachungaji watatu wabaya. Tena uvumilivu wangu kwa kondoo ukaniishia, nao kwa upande wao, wakanichukia.
9 Basi, nikawaambia, “Sitakuwa mchungaji wenu tena. Atakayekufa na afe! Atakayeangamia na aangamie! Na wale watakaobaki na watafunane wao kwa wao.”
10 Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa.
11 Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu.
12 Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu.
13 Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.” Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu.