3 Siku hiyo nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama jiwe zito kwa watu wote: Yeyote atakayelinyanyua atajiumiza mwenyewe. Watu wa mataifa yote duniani wataushambulia mji huo.
4 Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitamtia hofu kila farasi, na mpandafarasi wake nitamfanya kuwa mwendawazimu. Farasi wa mataifa mengine nitawapofusha. Lakini kabila la Yuda nitalilinda.
5 Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’.
6 “Siku hiyo, viongozi wa Yuda nitawafanya kama chungu cha moto mkali katika msitu; naam, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watayateketeza mataifa yote yaliyo kandokando yao. Lakini watu wa Yerusalemu wataendelea kuishi salama katika mji wao.
7 “Nami Mwenyezi-Mungu nitawasaidia kwanza jamaa za Yuda kusudi wazawa wa Daudi na wakazi wa Yerusalemu wasijione kuwa maarufu zaidi ya watu wengine wa kabila la Yuda.
8 Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawalinda wakazi wa mji wa Yerusalemu; walio wanyonge zaidi miongoni mwao watakuwa na nguvu kama mfalme Daudi. Wazawa wa Daudi watashika usukani kuwaongoza watu wa Yuda kama malaika wangu mimi Mwenyezi-Mungu, naam, kama mimi Mungu mwenyewe.
9 “Siku hiyo, nitayaangamiza mataifa yote yanayotaka kuushambulia mji wa Yerusalemu.