29 Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?
30 Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing’arazo,
31 akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
32 Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.
33 Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.
34 Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
35 bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.