12 Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi.
13 Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa BWANA;
14 akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina!
15 Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa BWANA.
16 Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko.
17 Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya BWANA na mfalme na watu, ili wawe watu wa BWANA; tena kati ya mfalme na watu.
18 Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunja-vunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka maakida juu ya nyumba ya BWANA.