1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha.
3 Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote.
4 Naye Yehoahazi akamsihi BWANA, BWANA akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa.
5 (BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza.
6 Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria).
7 Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa.