9 Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.
10 Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?
11 Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda.
12 Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.
13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, mikono mia nne.
14 Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.
15 Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?