16 Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la BWANA, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru.
17 Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na amiri wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.
18 Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.
19 Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?
20 Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?
21 Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.
22 Lakini mkiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu?