10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.
11 Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.
12 Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini.
13 Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone.
14 Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie.
15 Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme.
16 Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA.