20 ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa.
21 Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
22 Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu;
23 basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
24 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu;
25 basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao.
26 Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo;