3 Tena itakuwa katika siku ile, ambayo BWANA atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa;
4 utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema,Jinsi alivyokoma mwenye kuonea;Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri!
5 BWANA amelivunja gongo la wabaya,Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.
6 Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu,Kwa mapigo yasiyokoma;Aliyewatawala mataifa kwa hasira,Ameadhibiwa asizuie mtu.
7 Dunia yote inastarehe na kutulia;Hata huanzilisha kuimba.
8 Naam, misunobari inakufurahia,Na mierezi ya Lebanoni, ikisema,Tokea wakati ulipolazwa chini wewe,Hapana mkata miti aliyetujia.
9 Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako,Ili kukulaki utakapokuja;Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako,Naam, walio wakuu wote wa dunia;Huwainua wafalme wote wa mataifa,Watoke katika viti vyao vya enzi.