9 Basi, naililia mizabibu ya Sibma kwa kilio cha Yazeri, nitawanyeshea machozi yangu, Ee Heshboni na Eleale, kwa kuwa kelele za vita zimeyaangukia mavuno ya matunda yako, na mavuno ya mizabibu yako.
10 Na furaha imeondolewa, na shangwe toka mashamba yaliyozaa sana; hapana kuimba katika mashamba ya mizabibu, wala sauti za furaha; akanyagaye hakanyagi divai katika mashinikizo; nimeikomesha sauti ya furaha yake akanyagaye.
11 Kwa sababu hiyo mtima wangu unamlilia Moabu kama kinubi, na matumbo yangu kwa ajili ya Kir-Heresi.
12 Tena itakuwa, Moabu akionekana, na kujichosha kwa kulia juu ya mahali pa juu, na kuingia katika patakatifu pake aombe, hatapata kushinda.
13 Hilo ndilo neno lile alilolisema BWANA juu ya Moabu zamani.
14 Lakini sasa BWANA asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, pamoja na wingi wake wote; mabaki yake yatakuwa machache sana, kama si kitu kabisa.