1 Ole wa taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai!
2 Tazama, Bwana ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, tufani iharibuyo, kama dhoruba ya maji mengi yafurikayo, ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono.
3 Taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu itakanyagwa kwa miguu;
4 na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa hari, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake.
5 Katika siku ile BWANA wa majeshi atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake.
6 Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni.
7 Lakini hawa nao wamekosa kwa divai, wamepotea kwa kileo; kuhani na nabii wamekosa kwa kileo, wamemezwa kwa divai, wamepotea kwa kileo; hukosa katika maono, hujikwaa katika hukumu.