2 mtu hodari na mtu wa vita; mwamuzi na nabii; mpiga ramli na mzee;
3 jemadari aliye juu ya watu hamsini, na mtu mstahifu, na mshauri, na fundi aliye mstadi, na mganga ajuaye uganga sana.
4 Nami nitawapa watoto kuwamiliki, na watoto wachanga kuwatawala.
5 Nao watu wataonewa, kila mtu na mwenziwe, na kila mtu na jirani yake; mtoto atajivuna mbele ya mzee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima.
6 Mtu atakapomshika ndugu yake ndani ya nyumba ya baba yake, akisema, Wewe una nguo, ututawale wewe; na mahali hapa palipobomoka pawe chini ya mkono wako;
7 basi, siku ile atainua sauti yake, akisema, Mimi sitakuwa mponya watu; kwa maana ndani ya nyumba yangu hamna chakula wala mavazi; wala hamtanifanya kuwa mtawala juu ya watu hawa.
8 Kwa maana Yerusalemu umebomolewa na Yuda wameanguka, kwa sababu ulimi wao na matendo yao ni kinyume cha BWANA, hata wayachukize macho ya utukufu wake.