19 Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti?
20 Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?
21 Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi.
22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.
23 Imbeni, enyi mbingu, maana BWANA ametenda hayo;Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi;Pazeni nyimbo, enyi milima;Nawe, msitu, na kila mti ndani yake.Maana BWANA amemkomboa Yakobo,Naye atajitukuza katika Israeli.
24 BWANA, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?
25 Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;