9 Kwa sababu hiyo hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! Latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu.
10 Twapapasa-papasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao waliowanda tumekuwa kama wafu.
11 Sisi sote twanguruma kama dubu; twaomboleza kama hua; twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi.
12 Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua;
13 katika kukosa na kumkana BWANA, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni.
14 Na hukumu imegeuka ikaenda nyuma, na haki inasimama mbali sana; maana kweli imeanguka katika njia kuu, na unyofu hauwezi kuingia.
15 Naam, kweli imepunguka kabisa, na yeye auachaye uovu ajifanya kuwa mateka; naye BWANA akaona hayo, akachukizwa kwa kuwa hapana hukumu ya haki.