9 Nami nitaleta uzao toka Yakobo, na mrithi wa milima yangu toka Yuda, na mteule wangu atairithi, na watumishi wangu watakaa huko.
10 Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng’ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.
11 Bali ninyi mmwachao BWANA, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandika meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;
12 mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu nilipoita hamkuitika; niliponena, hamkusikia; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.
13 Kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa; tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika;
14 tazama, watumishi wangu wataimba kwa furaha ya moyo, bali ninyi mtalia kwa huzuni ya moyo; mtapiga kelele kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
15 Nanyi mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa wateule wangu. Na Bwana MUNGU atakuua; naye atawaita watumishi wake kwa jina lingine.