24 Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.
25 Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma.
26 Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao.
27 Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza, nawe utawaita; lakini hawatakuitikia.
28 Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya BWANA, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.
29 Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe,Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima;Kwa maana BWANA amekikataa na kukitupaKizazi cha ghadhabu yake.
30 Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema BWANA; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.